1. Isa42:
1-4,6-7
|
2. Mdo
10:34-38
|
Injili: Mt
3:13-17
|
" Daima tufanywe viumbe wapya katika Kristo kwa
njia ya ubatizo wetu"
Kuna kisa cha mtu mmoja
aliyeenda kwa muuza nguo na mshona nguo, aliingia mahali pale na kuangaza
kuzunguka katika hilo duka la muuza nguo kwa kuangalia mavazi mbalimbali
yaliyokuwemo mle dukani, na baadaye huyo mtu ambaye umri wake kidogo ulikuwa ni
umri wa uzee alirudi kwa huyo muuza nguo na kumwambia, tafadhali naomba
unitengezee vazi zuri la kike namna ya mkaja lakini lisiwe kubwa liwe dogo
kiasi, maana kesho ni siku ya mjukuu wangu. Huyo mtu aliendelea kubainisha kuwa
lile vazi lilikuwa kwa ajili ya mjukuu wake.
Mtengeneza nguo alipata
kuwa na shahuku ya kujua umri wa huyo aliyekuwa akiombewa na Babu yake
atengenezewe hiyo nguo maalum, " mjukuu wako ana miaka mingapi?",
mzee alijibu," hadi sasa ninapoongea hii ni siku ya saba tangia
azaliwe" mtengeneza nguo alibaki ameduwaa kwa kuwa hilo lilikuwa siyo
jambo la kawaida. Hivyo huyo mzee aliendelea kusisitiza hilo vazi litengenezwe
vizuri kwa kusema, " hakikisha hilo vazi linapendeza, maan kesho ni siku
ambapo mjukuu wangu ni siku yake yakukutana na Mungu" kwa mshangao yule
muuza nguo aliendelea kuwa na wasiwasi, kwa kumuuliza tena yule mzee kwa
mshangao," kukutana na na Mungu?? mzee alijibu, " kesho ni siku yake
ya kubatizwa"
Wengi wetu hata kama
siyo wote tulibatizwa tukiwa bado wadogo sana kiasi kwamba saa nyingine huwa
inatuwia vigumu kukumbuka ile siku muhimu katika maisha yetu ambapo tulibatizwa
na tukawa wana wa Mungu. Hatuwezi kukumbuka na kujua ni namna gani siku ya
ubatizo wetu wazazi wetu, wazazi wetu wa ubatizo walivyokuwa wanajibu maswali
na kukiri imani kwa niaba yetu?? Huu ndoo wakati ambapo tulipata majina yetu
kwa njia ya ubatizo.
Leo ni siku ambayo
tunafanya sherehe ya ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristu, twaweza jiuliza maswali
mengi sana juu ya kwanini Yesu alipata kubatizwa kule mto Yordani? Sakramenti ya ubatizo maana yake huwa ni
kuondoa dhambi ya asili, hivyo twaweza jiuliza kuwa hivi Yesu alibatizwa kwa
kuwa alikuwa na dhambi ya asili pia? Jibu ni kwamba hakuwa na hiyo dhambi ya
asili, na kwa kubainisha hilo mtakatifu Ambrozi mwalimu wa Kanisa alikuwa na
haya ya kusema juu ya ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristu: "
Bwana wetu Yesu Kristu alibatizwa si kwa sababu ya dhambi ya asili, bali
alibatizwa ili akayasafishe na kuyatakasa maji ili yawe
na
nguvu ya ubatizo"
Ni kwa msingi huo tunaona Kristu
anabatizwa ili apate kuunganika na sisi katika ubinadamu wetu uliodhaifu hasa
akiungana nasi katika ile safari yetu ya hija ya ufalme wa mbinguni. Hivyo yupo
nasi na ni mmoja wetu. Kila mmoja
wetu atambue amezaliwa na dhambi ya asili, Kanisa ni chombo cha Mungu ambapo
hiyo dhambi ya asili huondolewa na hivyo sisi kuitwa watoto wa Mungu. Naye
mtakatifu Vincent Ferrer alikuwa na haya ya kusema juu ya ubatizo; " kila mkristu mbatizwa inabidi
atambue kuwa ni ndani ya tumbo la Kanisa kila mmoja wetu hugeuzwa kutoka kuwa
mwana wa Adamu kuwa mwana wa Mungu."dhambi ya adamu iliyofanya wote
tukawa na dhambi ya asili, hiyo dhambi ya asili huondolewa na nguvu ya
sakramenti ya ubatizo na hivyo kutufanya tusiwe chini ya uvuli wa Adamu, bali
tuwe viumbe wapya katika Kristu.
Ubatizo kwetu maana
yake ninini?ubatizo ni sakramenti tuipokeayo, ambayo hutuosha dhambi ya asili
na hatimaye sisi huitwa wana wa Mungu. Daima ili tuwe wana wa Mungu ni lazima
sote tushiriki ule ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristu. Kristu anavyobatizwa ni
kiashilio cha kuanza kwa utume wake, ni kiashilio cha kutangaza ufalme wa
mbinguni hapa duniani, wengine waliozoea lugha ya wanasiasa utasikia hapa na
pale wanasema neno, ' sela' na vivyo hivyo kwa ubatizo Kristu mwenyewe
anajiweka wakfu kwa ajili ya kazi aliyotumwa kufanya duniani, na kazi kubwa
kuliko zote ilikuwa ni kuutangaza ufalme wa Mungu kwa mataifa na vizazi vyote.
Kwa njia ya ubatizo
tunazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Tunakuwa tumetakaswa kutoka dhambi
ya asili na hivyo tunakuwa wana wa Mungu. Kwa njia ya ubatizo huwa ndo
tunaingizwa Kanisani na kuwa moja ya jamii ya wakristu wanaounda kanisa
duniani. Hii hatua ya kuingizwa kanisani kwa waliobatizwa yaweza fananishwa na
moja ya mila zetu ambapo mmojawapo akitaka kuhesabiwa kuwa ni mmoja wa wanaukoo
fulani katika jamii husika, hupitia hatua iitwayo jando( initiation- rites of
passages) sasa nasi wakatoliki tuko sambamba na lile lifanyikalo katika
tamaduni zetu, sisi jando yetu huwa ni kumwandaa mtoto/mkatekumeni kwa hatua
ili aweze kupokelewa kanisani na hatimaye kuwa mwanajumuiya kamili wa kanisa
linaloungama imani moja.
Sakramenti ya ubatizo
ni alama na ishara inayotukumbusha kuwa tumejiweka wakfu katika ufalme wa Mungu.
Kupitia ubatizo ni dhahiri kuwa huwa tunakuwa tayari kumtumikia Mungu kama
manabii, wafalme, na makuhani. Kwa njia ya sakramenti ya ubatizo huwa
tunaimarishwa pia na roho mtakatifu, kwani ile siku ambayo kila mmoja wetu
hubatizwa humpokea roho mtakatifu pia. Huyo roho mtakatifu tumpokeaye wakati wa
ubatizo ni yule roho ambaye hutupa nguvu za kupambana na vishawishi na pia
kupambana na magumu mbalimbali.
Juu ya nguvu ya
Sakaramenti ya ubatizo Papa Benedict xvi alikuwa na haya ya kusema, " thamani ya ubatizo ni
msingi imara wa umissionari kwa kila mmoja wetu aliyebatizwa, kwa kuwa yule
ambaye amependa kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya ubatizo ni lazima afuate
nyayo zake yule aliyemshuhudia kwa njia ya matendo. Hivyo kwa njia ya ubatizo
tumekuwa warithi katika kufanya kazi ya Bwana kwa njia ya umissionari."
Kwa kumalizia hebu
tuangalie zile sifa kuu za Kristu aliyebatizwa, je naweza kulinganisha hizo
sifa za Yesu mbatizwa na maisha yangu?
Yesu
alikuwa maskini lakini mimi siyo maskini.
Yesu
alikuwa mnyenyekevu na mtii, lakini mimi siyo mtii.
Yesu
alikuwa mpole, lakini mimi siyo mpole.
Yesu
alisamehe, lakini mimi naweka roho ya kulipiza visasi.
Yesu
alitii mamlaka, lakini mimi daima hutaka kutotii na saa nyingine kuwaamlisha
wengine kwa faida yangu.
Yesu
alichukiwa kwa sababu ya ukweli, mimi nauzika ukweli ili nipendwe zaidi na
nilinde maslahi yangu.
Yesu
alipaa mbinguni kwa njia ya mateso na msalaba, lakini mimi kwa upande wangu
nataka kufika huko kwa njia ya starehe na raha bila ya msalaba.
Je
hiyo ni sawa kuwa mtumishi awe hivyo kuliko yule mwalimu wake?
No comments:
Post a Comment