Saturday, 21 January 2017

MAHUBIRI JUMAPILI YA TATU YA MWAKA A KIPINDI CHA KAWAIDA


1. Isa 9:1-4
2.1Kor 1:10-13,17
Injili: Mt 4:12-23

            " Ili kupata samaki wazuri uvumilivu wahitajika"

Wapendwa katika Kristu, leo tunaadhimisha jumapili ya tatu ya kipindi cha kawaida cha mwaka ambapo katika masomo yetu hasa somo la Injili tunasikia Yesu anawaita wafuasi wake wa kwanza kabisa:  Peter, Andrea, Yakobo na Yohane ( Mt4:12-23). Hawa walioitwa kumfuata Kristu kazi yao kabla ya hapo ilikuwa ni kuvua samaki, lakini tunaona leo Yesu anawaita wawe wafuasi wake ili wawe ni wavuvi wa watu. Hawa ni kundi la watu ambao walikuwa na mtizamo na fikra za aina fulani katika maisha yao, lakini Kristu anatumia hiyo fursa ya huo mtizamo wao kuwa fursa yenye mtizamo zaidi ya ule mtizamo waliokuwa nao wale wavuvi wa samaki, huo mtizamo wa Bwana wetu Yesu Kristu kwa wale aliowaita wawe wafuasi na wanafunzi wake, ni mtizamo wa kutoka na kuingia ndani zaidi kwenye maisha ya watu baadala ya maisha ya viumbe vingine.


Ndugu wapendwa katika Kristu tunapata kujifunza kuwa Kristu anvyowaita hawa wafuasi wake wa kwanza kuacha kazi ya uvuvi na kumfuata ili wawe wavuvi wa watu, tunapata fundisho kuwa ziwa/ bahari daima kadiri ya tafsri ya maandiko matakatifu ni ishara ya uovu/ubaya, hivyo Kristu anavyowaambia kuwa waende duniani wakawavue watu, anagusia dhana ya watu waovu, na maovu yao duniani. Dunia tunayoishi imejaa mema na maovu pia, hii dunia yaweza pia chukua picha/taswira ya ziwa au bahari ambapo ziwani au baharini kuna aina mbalimbali za viumbe, wakiwemo samaki wa aina mbalimbali. Ni katika mtizamo huu tunaona Yesu anawaita hawa waende katika ile bahari kubwa sana ili waweze kuwavua watu, kwa maana ya kuwafundisha watu fadhila za Krikristu kutoka fadhila za kidunia.


Swali ambalo twaweza jiuliza na pia likapata kutuongoza katika tafakari yetu ni kwamba kwa nini Yesu anawaita hawa wavuvi? twaweza jibu hili swali tukiambatanisha sifa alizo nazo mvua samaki. Kwa msingi huu hizi ndoo sifa ambazo anazo mvua samaki Kristu anazitumia katika kutufikishia ujumbe wa Neno la Mungu. Hebu tuone hizo sifa:


Kwanza, mvua samaki ni mtu ambaye ana uvumilivu wa hali ya juu. Daima mvua samaki huwa na uvumilivu katika kufanya kazi yake ya kuvua akirusha ndoana au jalife bahari au ziwani au mtoni huwa anakuwa na subira hadi kuhakikisha kuwa samaki wanaingia katika hilo jalife. Ni kwa msingi huu twaweza baini kuwa katika kuwahubiri Neno la Mungu wale ambao bado hawajaipata habari njema ya wokovu, daima kunahitaji uvumilivu, maana watu hawawezi wakabadilishwa na mahubiri au tafakari ya siku moja, hivyo ni lazima na muhimu kuwa na uvumilivu katika kutangaza habari njema ya Bwana. Walisikialo neno la Bwana hupata kuelewa Neno, na kubadilika kufuatana na uvumilivu wa mchungaji.


Pili, mvua samaki daima huwa na ile sifa ya kutokata tamaa. Daima mvuvi akirusha ndoana baharini, hasipofanikiwa hurudia tena na tena hadi kuhakikisha kuwa anafanikiwa, hivyo kwetu ni fundisho kuwa katika maisha yetu ya Kikristu hatuhitaji kukata tamaa pale ambapo tunaona maisha yetu ya utume, maisha yetu kama wakristu hayaendi, au pale ambapo tunaona giza katika maisha ya ufuasi wa Bwana wetu  Yesu Kristu, daima kwa neema ya Mungu tunahitaji tuwe imara na tuwe na ile roho ya kutokata tamaa.


Tatu, mvua samaki huwa na ile sifa ya kuwa shupavu. Mvua samaki daima huwa yupo tayari kukumbana na mawimbi makali ya bahari au ziwa au mto, huwa tayari kuweka maisha yake mdomoni mwa wanyama wakali wa bahari kama vile Mamba, Nyangumi, viboko, nk hayo yote huyapitia ili aweze kupata anachohitaji kupata katika safari yake. Vile vile wahubiri, wachungaji daima hupata changamoto katika bahari ya maisha. Daima huwa ni changamoto kuwahubiria watu ukweli na wote wakaukubali ukweli. Hivyo daima ni dhahiri kuwa katika kuhubiri ukweli lazima yule atangazaye Neno la Mungu hupata changamoto za kutukanwa, au kukataliwa kwa sababu ya kusimamia ukweli wa Neno la Mungu. Yule ahubiriye ukweli ndoo yule atakaye chukiwa na ndugu zake, atakayetemewa mate na saa nyingine atakeye tukanwa na watu, yule asimamaye katika njia ya haki na ukweli daima huwa na marafiki wachache. Katika hili tunaalikwa kuuishi kuhubiri na kuishi ukweli.


Nne, mvuvi daima huwa ana akili ya kusoma alama za nyakati katika kutenda kazi yake.  Mvua samaki hujua kuwa haya ni majira ya kupata samaki wengi, na pengine hujua na kutabiri kuwa muda fulani siyo rahisi kuwapata samaki. Anajua ni lini arushe jarife baharini, au aweke ndoana baharini. Mvuvi anajua tosha kuwa siyo kila majira samaki wana patikana kwa wingi, bali yeye hujua majira ya kuwapata samaki wengi na majira ambapo samaki huwa daima ni wachache au saa nyingine hakuna kabisa. Hivyo katika kutangaza Neno la Bwana hatuna budi kusoma alama za nyakati na kutambua kuwa huu ni wakati wa watu kuukubali ujumbe wa Neno la Mungu, au hu ni wakati watu kutokubali kiurahisi Neno la Mungu. Ni kwa msingi huu twaweza baini muda wa kusikiliza{ kutafakri} na muda wa kuongea na watu.


Tano, mvuvi mwerevu huwa na anajua namna ya kutupa chambo baharini au ziwani ili apate kumpata samaki vyema. Mhubiri mzuri ni yule anayetambua kuwa hawezi  kuwavuta watu wote kwake, mtangaza Neno la Mungu, daima anahitaji kujua mazuri yake na mapungufu yake. Hivyo katika kutangaza Neno la Bwana daima tutambue kuwa kuna nyakati ambazo kile tukihubilicho kinaendana na maisha yetu wenyewe, na pia maisha ya watu tuwahubilio.


Mwisho, mvuvi mwerevu daima huwa anajitahidi kuficha kivuli chake pindi avuapo samaki, maana hasipoficha hicho kivuli hatofanikiwa kupata hata samaki mmoja. Vivyo hivyo muhubir mzuri na mwerevu hawahubiri au hatangazi Neno la Bwana kufuatana na hisia na vionjo vyake, bali muhubiri mwema na mzuri  huwahubiria watu maisha Kristu. Mhubiri mwema daima huvaa utu na sura Kristu. Mhubiri ni Kristu mwingine katika kuwafanya watu walielewe neno la Mungu. Lengo la mhubiri daima ni kuwafanya watu waweke macho na mioyo yao kwa Kristu kuliko kuwafanya watu wahamishie mioyo na macho yao kwake ( kuishi maisha yenye kupendeza, maisha yenye kumbeba na kumpeleka Kristu kwa wengine).


Ndugu wapendendwa twaweza tambua kuwa kila mmoja wetu ameitwa na Bwana katika kumtumikia, hivyo ni mwaliko kwetu sote kutumia kalama zetu, na mapaji yetu tuliyojaliwa na Mungu katika kuhubiri Neno la Bwana. Kila mmoja anaitwa na Kristu na kutumwa na Kristu kuwa mmisionary pale alipo. Lile lolote ambalo kila mmoja wetu afanyalo alifanye kwa utukufu wa Bwana kwani ni huyo Bwana ambaye hutoa kwa kila mmoja wetu kadiri ya mapenzi yake.


                                                                                                      

No comments:

Post a Comment