1. Isa.60: 1-6
|
2.Ef 3:2-3,5-6
|
Injili: Mt 2:1-12
|
"
Hata asili yaweza kuongea na kumpeleka
mtu kwa Mungu"
Ndugu zangu basi
niwaalike tuweze kutafakari Neno la Mungu pindi tunapoadhimisha Jumapili ya
tokeo la Bwana wetu Yesu Kristu yaani, Epifania.
Katika masomo yetu hasa
somo la injili twaweza baini kuwa katika safari yetu ya imani kuna aina tatu za
watu; wale ambao humtafuta Mungu na kumtumikia; wale ambao wanamtafuta Mungu
lakini bado hawajamwona; na mwisho wale ambao hawana haja/shauku ya kumtafuta
Mungu. Kundi la kwanza la aina ya watu wamtafutao Mungu ni lile kundi la watu
wenye amani na furaha, kundi la pili ni lile kundi la watu wenye uso wa huzuni
kwa sababu wanamtafuta Mungu lakini hawajamwona katika maisha yao, nalo kundi
la tatu ni kundi la wajinga, yaani wale ambao hawana hata hamu ya kukutana na
Mungu mwumba wao.
Tunaona hizo aina tatu
za wale wamtafutao Mungu kama inavyodhihirishwa katika masomo yetu, hebu tuone
aina mojawapo, ambayo hii ni aina ya tatu ya wale wamtafutao Mungu, yaani kundi
la wajinga ambao hawa daima hujifanya wanamtafuta Mungu kumbe ndani yake wana
hila ya kufanya maovu kwa kutumia hiyo nafasi. Basi ni kwa msingi huu twaweza
sema kuwa aina hii ya tatu kadiri ya somo la injili inaangukia kwa mfalme
Herode, huyu anajifanya kumtafuta Mungu kumbe anazo hila nyingi ndani yake,
yeye lengo lake ilikuwa kutafuta kumwua Yesu ili apate kulinda madaraka yake
yasipokonywe na huyo mfalme aliyezaliwa. Tunaambiwa kuwa mfalme Herode kwa
kusutwa na dhamila yake mbaya anaamua kuwa ua hata watu wa familia yake akiwemo
mke wake Mariamme na watoto wake wawili. Herode kimsingi anawakilisha kundi la
watu ambao hutumia madaraka vibaya, watu ambao hujifanya wako karibu na Mungu
kumbe wana malengo mengine.
Pia tunaona kundi
jingine la wale wamtafutao Mungu na kukutana naye na hatimaye kumtumikia, basi
hili siyo kundi jingine bali ni Yosefu na Maria, na pia katika hilo kundi
twaweza kujumuisha wale wachungaji( Lk2:8-12). Hivyo ni kwa msingi huu twaweza
sema kuwa hili ni kundi lenye amani na furaha kwa kuwa wamekumkutana na Mungu.
Kundi jingine la watu
wamtafutao Mungu, ni Mamajusi, hawa ni wale wamtafutao Mungu kwa nguvu zao zote
na juhudi zao zote bila ya kuchoka. Mamajusi ni neno ambalo lina msingi wake
kutoka lugha ya Kigiriki " Magoi" ambapo nalo hilo limezaa neno la
kiingereza, " magic" au " magician" hawa mamajusi walikuwa
siyo wachawi kama tuwaonao kwenye mazingira yetu, bali hawa walikuwa ni
wataalamu wa nyota, na hivyo katika ufumbuzi wao walikuwa wakitaka kujua
uhusiano uliopo kati ya nyota na dunia. Hawa kwa ujuzi na utaalamu wao waliitwa
watu wa hekima kwa kuwa wao walifuata alama za asili na hizo alama za asili
ziliwaongoza hadi kwa Kristu.
Kwa upande wetu ni
nyota ipi ambayo inaweza tupeleka kwa Kristu? Je mimi ni nyota ya kumpeleka
mwingine kwa Kristu? Ni nyota ipi ya kwanza ambayo ilikupeleka wewe kwa Kristu
Yesu?? Jibu ni kwamba ile nyota ya kwanza ambayo ilinipeleka mimi na
ikakupeleka kwa Kristu Yesu ni wazazi wetu/ walezi wetu pindi tulivyokuwa wadogo
au tukishakuwa watu wazima, tukiikumbuka ile siku yetu ya kwanza tulipobatizwa
na kuitwa wana wa Mungu katika Yesu Kristu mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.
Wazazi wetu/ au walezi wetu, au malezi mazuri ya Kikristu na elimu ya maandiko
matakatifu, walimu na watu wenye maarifa mbalimbali, kwa msingi huo twaweza sema
kuwa, hizo zote ni nyota ambazo
zimetupeleka kwa Kristu na hizo ndoo nyota ambazo zinatuongoza hadi kwa Kristu
hadi leo hii.
Mamajusi walimpelekea
Yesu dhahabu, uvumba, na manemane,zikiwa ni alama za mali asili za dunia. Hata
hivyo kwa upande wetu sisi hatuna haja ya kumpelekea Mungu dhahabu, manemane,
na uvumba, baadala yake sisi Yesu tunampelekea Mioyo yetu, akili zetu na utashi
wetu wa kumtumikia na kukaa naye daima, hizo kimsingi ndoo zawadi zetu kubwa
kwa Yesu Kristu. Dhahabu, uvumba na manemane vyaonekana kuwa vilikuwa ni vitu
vya thamani sasa kwa wakati ule hata hadi nyakati zetu.
Hawa mamajusi kwa
kubeba hivyo vitu na kumpelekea Kristu ni fundisho kwetu kuwa hawa, wanatupa
ishara ya kuacha mali dunia, kuacha mambo mengi ya dunia yenye thamani na kisha
kumtafuta Kristu na hatimaye kuweza kukaa naye. Sisi upande wetu nasi twaweza
labda jiuliza swali moja kubwa kuwa ni vingapi tulivyo navyo kama vile utajiri,
hela na mali nyinginezo zinatuzuia kwenda kwa Kristu? hawa mamajusi wametumia
huo utajiri ili uweze kuwafikisha kwa Kristu.
Kumbe kwetu nasi hili
liwe somo na fundisho kuwa vile vyote tulivyonavyo kama mali, utajiri na
vingine vingi, basi kumbe twaweza vitumia kama njia ya kutufikisha kwa Yesu
Kristu. Mfano kama unamiliki gari, basi hilo gari litumie liwasaidie watu
baadala ya kuleta matatizo, kama una miliki simu ya kisasa, tumia hiyo nafasi
ya kumiliki hiyo simu katika kuinjilisha na kumtangaza Kristu baadala ya
kutumia hiyo simu kutenda maovu, kama una akili nyingi, basi itumie hiyo akili
uwasaidie watu wapate kumfikia Kristu kwa urahisi, kama wewe ni daktari basi
tumia hicho kipaji cha utabibu ili uwape watu maisha baadala ya kuwaondolea
maisha, kama wewe ni mwalimu, basi wafundishe watu mambo mazuri na njia njema
za kufika kwa Kristu, na kama wewe ni padre, askofu, mchungaji, basi tumia hiyo
kalama yako ya huo uchungaji ili uwavute watu kwa Kristu Yesu. Ni kwa msingi huo mimi naweza sema kuwa pia ni
mamajusi na wewe ni mamajusi wa kupeleka tulichonacho kwa Kristu na kubaki naye
daima.
Nimalizie tafakari hii
kwa kisa hiki: Kulikuwa na mtu mmoja ambaye alifanya kazi katika kiwanda cha
pamba, huyu alikuwa ni mkristu aliyejiwekea utaratibu wa kutokula nyama siku za
ijumaa akiendelea kutafakari mateso ya Kristu msalabani. Huyu daima siku za
ijumaa alibeba mayai na samaki kidogo kwa ajili ya mlo wake pindi awapo kazini.
Hivyo wafanyakazi wenzake ambao walikuwa siyo wakatoliki walimtania na
kumbatiza jina la " Bwana mayai na masamaki" wakati wao siku zote
walikuwa wakila wali kwa nyama. Na mbali ya kutaniwa na kufanyiwa kejeli za
namna hiyo, huyo ndugu hakuacha ule utaratibu wake wa kubeba hicho kitoweo
chake siku za ijumaa.
Huyo mtu miaka baadaye
alipata kukutana na mtu mmoja ambaye alikuwa amevalia mavazi ya upadre akitokea
Kanisani, hao wawili walipata kutambuana na hivyo kupata kuhabarishana mambo
mengi sana.
Hapo baadaye huyo padre aliyekuwa akitoka mlango wa Kanisa
alimwambia yule ndugu: " Ilikuwa ni mfano wako mzuri ndoo ulinifanya
niingie ukatoliki. Nilikumbuka zile siku ambazo ulikuwa unabeba samaki na mayai
kazini kwako na pia ukaanza kudhalauliwa na kuchekwa na ndugu zako uliofanya
nao kazi, lakini na mbali ya hayo madharau hukuacha/ kuikana imani yako, na
umedumu kwa kuilinda imani yako, nami kwa kuona hivyo nikaamua kujiunga na ukatoliki
maana nilifikiri sana kuwa kama huyu amedharauliwa namna hiyo na akazidi kuishi
na kuilinda imani yake, vivyo ni lazima kutakuwa na kitu cha pekee kwa
wakatoliki. Ni kwa jinsi hiyo niliamua kufuata imani ya Kanisa Katoliki. Leo
nimeadhimisha misa yangu ya kwanza ya Shukurani." huyo padre alimalizia
kutoa ushuhuda wake kwa huyo ndugu.
Epifania
maana yake ni kumdhihirisha Kristu, kumfunua Kristu kwa wale ambao bado
hawajapata kutambua uwepo wake katika maisha yao. Kwa kuwainjilisha watu kwa
mifano bora hasa kupitia maisha yetu tunavyoishi, ni dhahiri kuwa sisi tunakuwa
ni nyota za kuwapeleka watu kwa Kristu.
Tutabaki kujiuliza hili
swali kuwa je mimi ni nyota ya kuwapeleka watu kwa Kristu? Je kama ni nyota
nimewapeleka wangapi kwa Kristu? Daima tuwe nyota zenye mwanga wa kuwapeleka
watu kwa Kristu.
No comments:
Post a Comment