Isa 49:3; 5-6
|
2.1Kor 1:1-3
|
Injili:1:29-34
|
" Je na wewe ni
mwanakondoo?"
Wapendwa familia ya
Mungu tunaposheherekea jumapili ya pili ya kipindi cha kawaida cha mwaka wa
Kanisa tunaalikwa kutafakari juu ya Yesu kama mwanakondoo wa Mungu. Wazo kuu
ambalo litatuongoza katika tafakari yetu ni juu ya huyo mwanakondoo wa Mungu
kwetu ana maana gani na je twaweza kujifunza nini kutoka kwake huyo mwana
kondoo wa Mungu.
Katika Injili
tunamsikia mwinjili Yohane akigusia hili jambo kwa ukaribu, katika Injili
Yohane anasema, " tazama mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za
dunia"( Yohane1:29). Katika mazingira ya kawaida na uelewa wetu wa kawaida
pindi tusikiapo neno, " Mwanakondoo"
picha ambayo hutujia akilini mwetu ni juu ya yule mtu ambaye ni mpole
sana, mnyenyekevu, au yule ambaye hana sauti katika jamii. Lakini hata hivyo
tunapata motisha hapa kuwa Yesu alikuwa hana hiyo picha ya mwanakondoo kama
wengi ambavyo tunaweza fikiria. Baadala yake Yesu ni mwanakondoo ambaye amepewa
sifa ya kuondoa dhambi za dunia, hivyo huyo ni mwanakondoo mwenye nguvu, ni
mwanakondoo hasiye dhaifu, ni mwanakondoo ambaye yupo tayari kuufia ukweli.
Huyu ni mwanakondoo ambaye yupo tayari kubeba
hata lawama ili atimize mapenzi ya Mungu.
Kutoka katika maandiko
matakatifu twaweza pata picha mbili juu ya huyo mwanakondoo. Kwanza kabisa ni
kuwa huyo mwanakondoo damu yake inamwagika kwa ajili ya wengine. Hii taswira ya
huyo mwanakondoo ambayo mwinjili Yohane anatufundisha katika injili inapata
mizizi yake kutoka moja ya vitabu vya agano la kale. " Nao watatwaa baadhi
ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu katika
zile nyumba watakazomla."( Kut12:7) "
Kwa kuwa Bwana atapita
ili awapige hao wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha
juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha
mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu."( Kut 12: 23). Ni kwa msingi huo
tunapata ufahamu na uelewa juu ya hii taswira ya Yesu kama mwanakondoo kuwa
Yeye ajitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Ni kwa msingi huu twaweza sema juu ya
utumishi, kuwa yeyote ambaye anataka kuwa kiongozi lazima auvae ule utu wa
Kristu kama mwanakondoo. Yeyote ambaye ni kiongozi kwa maana ya kuwatumikia
watu, huyo hana budi kuitwa mwanakondoo. Kuwa kiongozi katika hii taswira/picha
ya mwanakondoo ni kukubali kukabiliana na hali zote yakiwemo magumu katika
kumfuasa Kristu mwanakondoo wa Mungu.
Mateso katika maisha yetu daima yatakuwa
ya msingi na ya maana pindi hayo mateso
yakitokana na utumishi wa kumtumikia Mungu. Yeyote yule ambaye anateseka
kwa ajili ya kumtumikia Mungu akiiga mfano wa yule mwanakondoo, kwake huyo
twaweza sema na bainisha kuwa anaishi yale mateso halisi ya Kristu msulubiwa.
Hivyo daima tukumbuke kuwa siyo kila shida, mateso/ mahangaiko katika maisha
twaweza yalinganisha na yale ya Kristu. Yule ambaye amejisababishia shida,
mateso kwa uzembe au kwa sababu ya kutenda dhambi hatuwezi sema kuwa hayo ni
mateso shirikishi katika yale mateso ya mwanakondoo wa Mungu. Mateso shirikishi
katika yale mateso ya mwanakondoo wa Mungu, ni yale mateso ambayo tunayashiriki
kwa ajili ya kuwa wafuasi kamili ya huyo mwanakondoo wa Mungu.
Tuna picha ya huyo
mwanakondoo wa Mungu ambaye daima yeye daima huwa siyo mwenye kulipa visasi na
kutumia nguvu dhidi ya maadui wake. Hii imedhihirishwa katika kitabu cha nabii
Isaia 53:7 " Alionewa, lakini yeye alinyenyekea, wala hakufunua kinywa
chake; kama mwanakondoo apelekwaye machinjioni, na kama vile kondoo anyamazavyo
mbele yao wakatao manyoya yake; Naam hakufunua kinywa chake." Hivyo ni
dhahiri kuwa hii picha ya mwanakondoo inatutafakarisha kuwa daima amani huwa
hailetwi kwa nguvu au suruba au kulipiza visasi, bali huletwa kwa fadhila ya
unyenyekevu na msamaha.
Tunapata picha pia ya
mwana-kondoo wa Mungu kuwa ni mtumishi asiye tafuta faida mbele ya wengine (
suffering servant) daima basi tutambue kuwa tunavyomtumikia Mungu,
tusitangulize faida au maslahi mbele kwani huyo Mungu aliyetuita tumtumikie
ndiye ajuaye namna na jinsi ya kuwalisha na kuwatunza wale ambao amewaita
wamtumikie. Daima hapa tunapata changamoto juu ya swala zima la uchungaji na
wachungaji wetu, kuwa daima hawa wachungaji kipau mbele cha kwanza katika
kumtumikia Mungu kwao nini? ni maslahi binafsi au ni kumtumikia Mungu bila ya
kuangalia hayo maslahi? hapo ni jukumu letu kujitafakari na kuiga huo mfano wa
mtumishi asiyetafuta faida au maslahi binafsi.
Tusisahau pia kuwa hii
picha ya mwana-kondoo kwetu sisi inagusia dhana ya ushindi. Basi kumbe huyu
mwanakondoo anayeongelewa ni anatupa habari njema ya ushindi. Kitabu cha ufunuo
kinabainisha huo ushindi ambapo inaelezwa kuwa, " wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa,
kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na
baraka." ( ufunuo5:12), " hawa
watafanya vita na mwana-kondoo, na Mwana kondoo atawashinda, kwa maana yeye ni
Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio
walioitwa, na wateule, na waaminifu.( ufunuo17:14) hivyo twaweza tambua
kuwa huyo mwana-kondoo tunayeelezewa habari habari zake kwa unyenyekevu wake
anajitwalia mamlaka, uweza na ushindi.
Ni kwa msingi huu
twaweza baini kuwa wakati wa ibada ya misa takatifu hasa tukifika kile
kipengere cha mwanakondoo wa Mungu( Agnus Dei), huwa tunaimba utenzi wa
mwanakondoo au kama siyo kuimba huwa tunatamka maneno yake. na wakati huo
kuhani huwa anachukua kipande cha mkate ulio altareni na kukivunja. Juu ya hilo
tendo Mtakatifu Yohane Chrisostom ( 407) alikuwa na haya ya kusema, " Kwa
kile ambacho Kristu hakukitesekea msalabani, anateseka kwa hii sadaka ya
ekaristi takatifu kwa ajili yenu." Hayo maneno huwa tunasikia daima padre
akiyarudia daima na daima pale ashikapo mwili wa Yesu na kusema maneno
yafuatayo, " huyu ndiye mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia
heri yao walioalikwa kwenye karamu ya Bwana..." Hivyo tunavyoadhimisha
ibada ya misa takatifu daima tunamwangalia yule mwana-kondoo aliyeteseka,
akafa, na akafufuka kwa ajili ya wokovu wetu. Daima yatupasa kuizunguka meza ya
Bwana kwa moyo wenye toba na unyenyekevu tukimwomba tuwe watumishi wake na
tumtumikie.
No comments:
Post a Comment