Tuesday, 31 January 2017

MAHUBIRI YA JUMAPILI YA TANO KIPINDI CHA KAWAIDA MWAKA A.


1. Isa 58: 7-10
2.1Kor2:1-5
Injili:Mt5:13-16

               " Tunaitwa kuwa chumvi na mwanga kwa dunia."

Wapendwa taifa la Mungu leo tunaadhimisha jumapili ya tano ya kipindi cha mwaka wa Kanisa. Katika kusheherekea jumapili hii, wazo muhimu na wazo kuu litakalotuongoza katika ibada yetu, ni kuwa sote kama wabatizwa wana wa Mungu tunaalikwa kuwa ' chumvi na mwanga kwa dunia'.

Masomo yetu ya leo hasa somo la injili linagusia maisha yetu katika ujumla wake hasa somo linagusia sisi kuwa kielelezo na mfano kwa wale ambao bado hawana maisha na fadhila za kikristu. Jumapili iliyopita tulisikia juu ya heri nane ambazo zilikuwa taratibu kwa yeyote yule kuingia katika ufalme wa mbinguni. Leo hii tunafundishwa juu ya kuwa mwanga na chumvi kwa ulimwengu ili tupate kuwavuta wengine na kuwafanya wakutane na Kristu.

Bwana wetu Yesu Kristu anatumia mfano wa chumvi na mwanga. Hii ni mifano halisi inayokubalika moja baada ya nyingine kadiri tunavyofahamu matumizi ya chumvi na mwanga. Kama chumvi ikiachwa bila kutumiwa kwenye chakula, hiyo chumvi haitokuwa na maana ya matumizi yake. Kama taa ipo lakini haiwezi ikaangaza mahala palipo giza ili watu wapate kuona vizuri, hiyo taa pia haitokuwa na maana kamwe. Chumvi pale inapowekwa kwenye chakula hutambulika uwepo wake maana hiyo chumvi huwa kikolezo cha radha katika chakula. Taa pia itatambulika umuhimu wake pindi ikiwashwa na kuwaangazia watu ili wapate kuona vyema.

Katika tafakari yangu basi nitatafakari nanyi nyote juu ya zile sifa kuu muhimu za chumvi nikizilinganisha na maisha yetu wakristu.

Kwanza, chumvi ikiwekwa kwenye chakula huwa inafanya chakula kinakuwa na radha ya aina yake. Kwa wale tutumiao chumvi katika chakula tunafahamu ni kwa jinsi gani na namna gani chakula hupoteza radha na hata hupoteza hamu kwa mlaji pindi ikikosekana chumvi. Vivyo hivyo kwetu sisi wakristu tunawajibu wa kuwa chumvi ( mifano bora kwa wengine) kadiri ya maisha yetu. Maisha yetu ni ushuhuda wa Kristu kwa wale ambao hawajampokea Kristu. Maneno yetu, mawazo yetu, matendo yetu hivyo vyote ni vielelezo ambavyo vyaweza kuwavuta wengine kwa Kristu Yesu. Maisha yetu ni injili inayomhubiri Kristu hata kwa wale wenzetu ambao siyo wakristu. Mawazo, maneno, na matendo yangu, ni karamu moja nzuri ya kuandika ujumbe wa Kristu katika maisha na mioyo ya wengine. Tukikaa wakristu jina hatutokosa kufananishwa na ile chumvi ambayo ipo ila haitumiki.

Pili, chumvi hufanya kazi ya kutunza chakula kisiharibike. Kabla ya kuja uvumbuzi wa vifaa vya umeme vyenye kuhifadhi vyakula visiharibike ( fridge) zamani mababu na mabibi zetu, japo hata leo hii njia yawezekana bado ikawa bado ipo, walitumia chumvi katika kuhifadhia chakula chao, kama vile nyama na vyakula vingine vingi ambavyo viliweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu kwa kutumia chumvi. Kwa upande wetu wetu wakristu tunakumbushwa na huo mfano kuwa ni kwa jinsi gani twaweza tunza tunu na fadhila zetu za kikristu siku zote za maisha yetu. Maisha ya ufuasi wa Kristu yana maana kubwa pindi zile tunu na fadhila zake zikiwa kama kielelezo na ngao yetu na utambulisho wetu katika maisha yetu kama wafuasi wake Kristu.

Tatu, chumvi huleta kiu. Twaweza jiuliza kitu kimoja kuwa ni mara ngapi maisha yetu kama wakristu yamekuwa ni chachu ya kuleta kiu kwa wengine ili wawe wafuasi pia wa Kristu? kwa maneno yake Kristu mwenyewe anabainisha: " Ninyi ni nuru kwa mataifa,"( Mt5:14). Katika dunia yetu leo ninini kinatokea na ninini kinaendelea? daima tunajikuta hatuna au hatutoi picha picha nzuri kwa ulimwengu kufuatana na mawazo, maneno na matendo yetu sisi wenyewe kutoendana na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristu. Kuna mtu mmoja ambaye amewahi kuwa maarufu duniani aliwahi sema haya maneno: " Ninampenda Yesu Kristu, ila siupendi ukristu," kuwa mafundisho ya Kristu ni mazuri sana yenye tunu na fadhila nzuri, ila sisi waumini tunapata changamoto moja kubwa kuwa zile tunu nzuri na fadhila za kikristu zinabaki vitabuni au kwenye maandishi tu bila ya kushuka ardhini.

Katika mikutano mbalimbali ya madhehebu ya wajiitao walokole daima tunapata changamoto kubwa sana tena sana kutoka kwa hao wainjilishaji wa Kilokole kwa kuwa wao daima humhubiri yule Yesu mtoa adhabu kali kwa yule asiyemwamini Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi! Binafsi sijui kama hii iko sawa au hapana. Labda nitaikubali hii tu pale ambapo watahubiri kwa kutoleta mashambulizi kwa madhehebu mengine au kwa kuwashambulia wengine kwa kuhubiri kwa mifano bora ya kuigwa kuliko kuhubiri kwa misimamo hasi peke yake.


Katika maisha yetu sisi kama wafuasi wa kristu bado tunakumbana na changamoto kubwa sana hasa kwa upande wa wachungaji ( watawa, mapadre, na maaskofu). Huwa ninini daima kinatokea pindi kuhani akianguka katika majaribu na dhambi? tumepata kushuhudia kuwa wapo makuhani ambao kwa madhaifu yao wameshindwa kulinda utu na heshima yao, wengi wameshuhudiwa tayari wakiwa ni walevi, na wengine kwa kuoa na kuzaa watoto na kutelekeza ile kazi waliyoitiwa na Bwana, hilo ni jambo ambalo katika uwazi na ukweli lipo na limekwisha kutokea. 


Changamoto kwetu sisi waumini tukiona hayo yanatokea kwa wale ambao wamewekwa tuwe chini yao huwa tunafanya nini? daima kitu ambacho huwa kinatokea kusambaza hayo matendo ya makuhani yasiyopendeza kwa wengine ikiwezekana hata kwa njia ya mitandao ya kijamii, kama vile whatsapp, facebook, youtube, twitter, n.k. Lakini kwa kuuliza swali moja tu la msingi ni kwamba, ni nani kati yenu aliwahi chukua muda wake akaaa chini na kuwafikiria hao wachungaji/ makuhani na akaamua kuwaweka kwenye sala na maombi ili basi roho mtakatifu azidi kutawala zaidi katika maisha yao na hatimaye wabadili mitizamo na mienendo yao?? ni mara ngapi waumini tumechukua nafasi kukaa karibu na hao wachungaji wetu na kuwa kitulizo kwao hasa kutokana na magumu wanayoyapitia kama binadamu wengine? kama ukikumbuka kuwaombea hao wachungaji wako basi wewe ni mwenye bahati, maana pia hao mapadre wako na maaskofu wako wanataka kusikia mazuri na kujifunza kutoka kwako wewe muumini, maana kila mmoja ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili awe chumvi na mwanga kwa mwingine.

No comments:

Post a Comment