1.
Isa 58: 7-10
|
2.1Kor2:1-5
|
Injili:Mt5:13-16
|
" Tunaitwa kuwa chumvi na
mwanga kwa dunia."
Wapendwa taifa la Mungu
leo tunaadhimisha jumapili ya tano ya kipindi cha mwaka wa Kanisa. Katika
kusheherekea jumapili hii, wazo muhimu na wazo kuu litakalotuongoza katika
ibada yetu, ni kuwa sote kama wabatizwa wana wa Mungu tunaalikwa kuwa ' chumvi
na mwanga kwa dunia'.
Masomo yetu ya leo hasa
somo la injili linagusia maisha yetu katika ujumla wake hasa somo linagusia
sisi kuwa kielelezo na mfano kwa wale ambao bado hawana maisha na fadhila za
kikristu. Jumapili iliyopita tulisikia juu ya heri nane ambazo zilikuwa
taratibu kwa yeyote yule kuingia katika ufalme wa mbinguni. Leo hii
tunafundishwa juu ya kuwa mwanga na chumvi kwa ulimwengu ili tupate kuwavuta
wengine na kuwafanya wakutane na Kristu.
Bwana wetu Yesu Kristu
anatumia mfano wa chumvi na mwanga. Hii ni mifano halisi inayokubalika moja
baada ya nyingine kadiri tunavyofahamu matumizi ya chumvi na mwanga. Kama
chumvi ikiachwa bila kutumiwa kwenye chakula, hiyo chumvi haitokuwa na maana ya
matumizi yake. Kama taa ipo lakini haiwezi ikaangaza mahala palipo giza ili
watu wapate kuona vizuri, hiyo taa pia haitokuwa na maana kamwe. Chumvi pale inapowekwa
kwenye chakula hutambulika uwepo wake maana hiyo chumvi huwa kikolezo cha radha
katika chakula. Taa pia itatambulika umuhimu wake pindi ikiwashwa na
kuwaangazia watu ili wapate kuona vyema.
Katika tafakari yangu
basi nitatafakari nanyi nyote juu ya zile sifa kuu muhimu za chumvi
nikizilinganisha na maisha yetu wakristu.
Kwanza, chumvi ikiwekwa
kwenye chakula huwa inafanya chakula kinakuwa na radha ya aina yake. Kwa wale
tutumiao chumvi katika chakula tunafahamu ni kwa jinsi gani na namna gani
chakula hupoteza radha na hata hupoteza hamu kwa mlaji pindi ikikosekana
chumvi. Vivyo hivyo kwetu sisi wakristu tunawajibu wa kuwa chumvi ( mifano bora
kwa wengine) kadiri ya maisha yetu. Maisha yetu ni ushuhuda wa Kristu kwa wale
ambao hawajampokea Kristu. Maneno yetu, mawazo yetu, matendo yetu hivyo vyote
ni vielelezo ambavyo vyaweza kuwavuta wengine kwa Kristu Yesu. Maisha yetu ni
injili inayomhubiri Kristu hata kwa wale wenzetu ambao siyo wakristu. Mawazo,
maneno, na matendo yangu, ni karamu moja nzuri ya kuandika ujumbe wa Kristu
katika maisha na mioyo ya wengine. Tukikaa wakristu jina hatutokosa
kufananishwa na ile chumvi ambayo ipo ila haitumiki.
Pili, chumvi hufanya
kazi ya kutunza chakula kisiharibike. Kabla ya kuja uvumbuzi wa vifaa vya umeme
vyenye kuhifadhi vyakula visiharibike ( fridge) zamani mababu na mabibi zetu,
japo hata leo hii njia yawezekana bado ikawa bado ipo, walitumia chumvi katika
kuhifadhia chakula chao, kama vile nyama na vyakula vingine vingi ambavyo
viliweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu kwa kutumia chumvi. Kwa upande wetu wetu
wakristu tunakumbushwa na huo mfano kuwa ni kwa jinsi gani twaweza tunza tunu
na fadhila zetu za kikristu siku zote za maisha yetu. Maisha ya ufuasi wa
Kristu yana maana kubwa pindi zile tunu na fadhila zake zikiwa kama kielelezo
na ngao yetu na utambulisho wetu katika maisha yetu kama wafuasi wake Kristu.
Tatu, chumvi huleta
kiu. Twaweza jiuliza kitu kimoja kuwa ni mara ngapi maisha yetu kama wakristu
yamekuwa ni chachu ya kuleta kiu kwa wengine ili wawe wafuasi pia wa Kristu?
kwa maneno yake Kristu mwenyewe anabainisha: " Ninyi ni nuru kwa
mataifa,"( Mt5:14). Katika dunia yetu leo ninini kinatokea na ninini
kinaendelea? daima tunajikuta hatuna au hatutoi picha picha nzuri kwa ulimwengu
kufuatana na mawazo, maneno na matendo yetu sisi wenyewe kutoendana na
mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristu. Kuna mtu mmoja ambaye amewahi kuwa
maarufu duniani aliwahi sema haya maneno: " Ninampenda Yesu Kristu, ila siupendi ukristu," kuwa mafundisho
ya Kristu ni mazuri sana yenye tunu na fadhila nzuri, ila sisi waumini tunapata
changamoto moja kubwa kuwa zile tunu nzuri na fadhila za kikristu zinabaki
vitabuni au kwenye maandishi tu bila ya kushuka ardhini.
Katika mikutano
mbalimbali ya madhehebu ya wajiitao walokole daima tunapata changamoto kubwa
sana tena sana kutoka kwa hao wainjilishaji wa Kilokole kwa kuwa wao daima
humhubiri yule Yesu mtoa adhabu kali kwa yule asiyemwamini Yesu kuwa ni Bwana
na mwokozi! Binafsi sijui kama hii iko sawa au hapana. Labda nitaikubali hii tu
pale ambapo watahubiri kwa kutoleta mashambulizi kwa madhehebu mengine au kwa
kuwashambulia wengine kwa kuhubiri kwa mifano bora ya kuigwa kuliko kuhubiri
kwa misimamo hasi peke yake.
Katika maisha yetu sisi
kama wafuasi wa kristu bado tunakumbana na changamoto kubwa sana hasa kwa
upande wa wachungaji ( watawa, mapadre, na maaskofu). Huwa ninini daima
kinatokea pindi kuhani akianguka katika majaribu na dhambi? tumepata kushuhudia
kuwa wapo makuhani ambao kwa madhaifu yao wameshindwa kulinda utu na heshima
yao, wengi wameshuhudiwa tayari wakiwa ni walevi, na wengine kwa kuoa na kuzaa
watoto na kutelekeza ile kazi waliyoitiwa na Bwana, hilo ni jambo ambalo katika
uwazi na ukweli lipo na limekwisha kutokea.
Changamoto kwetu sisi waumini
tukiona hayo yanatokea kwa wale ambao wamewekwa tuwe chini yao huwa tunafanya
nini? daima kitu ambacho huwa kinatokea kusambaza hayo matendo ya makuhani
yasiyopendeza kwa wengine ikiwezekana hata kwa njia ya mitandao ya kijamii,
kama vile whatsapp, facebook, youtube, twitter, n.k. Lakini kwa kuuliza swali
moja tu la msingi ni kwamba, ni nani kati yenu aliwahi chukua muda wake akaaa
chini na kuwafikiria hao wachungaji/ makuhani na akaamua kuwaweka kwenye sala
na maombi ili basi roho mtakatifu azidi kutawala zaidi katika maisha yao na
hatimaye wabadili mitizamo na mienendo yao?? ni mara ngapi waumini tumechukua
nafasi kukaa karibu na hao wachungaji wetu na kuwa kitulizo kwao hasa kutokana
na magumu wanayoyapitia kama binadamu wengine? kama ukikumbuka kuwaombea hao
wachungaji wako basi wewe ni mwenye bahati, maana pia hao mapadre wako na
maaskofu wako wanataka kusikia mazuri na kujifunza kutoka kwako wewe muumini,
maana kila mmoja ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili awe chumvi na mwanga
kwa mwingine.