1. Ybs :15:15-20
|
2.1Kor 2:6-10
|
Injili: Mt
5:17-37
|
" Kuchagua siyo shida, bali
shida ninini unachagua"
Katika moja ya hadithi
ambazo nimewahi zisoma, na hii ni mojawapo: Ilitokea wadhambi wawili
walimwendea padre ili wapate kuungama, walipofika kwa padre walikuwa na haya ya
kumwambia, " Baba padre tumefika hapa na tuko mbele yako, sisi ni
wakosefu, hivyo twahitaji msaada wako wa
sakramenti ya kitubio." Mmoja kati ya wale wadhambi alimwambia
padre kuwa yeye dhambi zake ni kubwa, na mwingine akamwambia padre kuwa dhambi
zake ni ndogondogo kiasi kwamba hajisikii kuziungama. Baada ya hayo maongezi
padre aliwaomba wote wawili walete mawe, kila mmoja alete mawe kadiri ya dhambi
zao walizotenda. Mmoja alienda akaleta jiwe moja kubwa sana, na mwingine
akaleta mawe mengi madogomadogo kwenye mfuko. Basi baada ya kupeleka hayo mawe
kwa yule padre, padre aliwaamuru pia kurudisha hayo mawe kila moja katika
nafasi lilipotoka jiwe. Yule aliyekuwa ameleta jiwe kubwa alijitahidi
kuliviringisha kadiri ya uwezo wake na kulirudisha mahala pake, na yule
mwingine aliyekuwa ameleta mawe madogomadogo kwenye mfuko, alianza kusumbuka na
kubabaika huku akikosa la kufanya, na baadaye alimwambia padre kuwa ilikuwa ni
vigumu kwake kuweza kukumbuka nafasi ya kila jiwe alipolitoa maana yalikuwa ni
mawe madogo sana kiasi kwamba alisahau hata nafasi za yale mawe yalipokuwa.
Baadaye yule padre aliweza kuwapa maana ya kile alichowaambia wakafanye. Padre
alisema kuwa, yule aliyeleta jiwe kubwa maana yake ni kwamba alikuwa na dhambi
kubwa sana ambapo ilichukua nafasi kubwa katika moyo wake, hivyo kwa kuishi na
hiyo dhambi hakukumpa raha kamwe bali daima alikaa akikumbuka kuwa lazima
akaungame hiyo dhambi na kutubu, na kwa yule aliyeokota mawe madogo madogo pia
padre alimwambia kuwa hayo mawe madogomadogo ni kielelezo cha dhambi ndogondogo
ambazo mbele ya fikra na macho ya binadamu huonekana kuwa hazina umuhimu wa
kuziungama na hivyo kuweza kusahulika kiurahisi sana. Hivyo huyo padre
alimalizia kwa kuwaambia kuwa wote wanahitaji kuungama na hatimaye kupata
huruma ya Mungu mbali ya kuwa na dhambi kubwa na ndogo. Padre alimalizia kwa
kusema kuwa dhambi ni dhambi na sakramenti ya kitubio ndoo yahitajika kuiondoa
hiyo dhambi.
Wapendwa katika masomo
yetu ya leo, katika injili tunapata habari njema ya Bwana wetu Yesu Kristu,
hasa juu ya ile hotuba aliyotoa mlimani akiwa na wafuasi wake. Hotuba hii
wengine huichukulia kama muhtasari wa mafundisho yake Bwana wetu Yesu Kristu.
Tumeanza kuisikia hiyo hotuba pale juu ya zile heri nane. Leo katika injili ya
mtakatifu Mathayo5:17-37, tunaambiwa namna dhambi itendwavyo, dhamira ya
kutenda dhambi, madhara na upotofu wa maadili utokanao na dhamira ya kutenda
dhambi.
Katika injili
tunafundishwa kuwa dhambi hutendwa kuanzia katika fikra iwapo mtu analengo la
kutenda uovu hata kama hatofanikiwa kuhalalisha uovu huo kimatendo basi hiyo
inahesabika kama dhambi, hata isipotendwa, kwa kuwa kinachoangaliwa hapa ni
dhamira au nia ya mtu. Mfano yawezekana mtu mmoja akawa na chuki na mtu
mwingine kiasi cha kudhamiria hata kumwondoa uhai, kadiri ya injili huo tayari
ni uuaji maana dhamira tayari ilikuwepo, hii ni sawasawa na uzinzi, maana
kitendo cha kutamani mwanamke au mwanaume tayari huo ni uzinifu ndani ya roho
ya yule atamaniye. Ni kwa msingi huu huwa daima katika ile sala ya nakuungamia
Mungu mwenyezi katika ibada takatifu ya misa huwa tunasema, "
..........nanyi ndugu zangu kwani nimekosa muno kwa mawazo, kwa maneno, na kwa
matendo..... hivyo hiyo ni dhahiri kuwa dhambi yaweza tendwa katika
hizo hali.
Katika Biblia tunasoma
kuwa, "kwa maana ndani ya mioyo ya
watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya,
ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo
maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi"(Mk7:21-23). Tunafundishwa
kutoka katika Biblia kuwa moyo wa binadamu ni chanzo cha yale yote ayatendayo
binadamu, ndani ya moyo wa mwanadamu yamejificha mengi sana. Ni katika msingi
huo tunaalikwa kuchagua yale yaliyo mema na kuacha yale mabaya, tunaalikwa
kuiga yale yaliyomema kutoka kwa wengine na siyo kuyaiga yale yaliyo mabaya
kwao. Katika kitabu cha Yoshua bin Sira tunaambiwa juu ya hayo pia kuwa, "
ukipenda utazishika amri zake na kutenda
amini ni shauri lako. Ameweka mbele yako moto na maji utanyosha mkono wako
uchaguavyo." Ybs15:15-16.
Dhambi maana yake
ninini? tunaambiwa kuwa dhambi ni matokeo ya kufanya kinyume na mapenzi yake
Mungu muumba wetu. Tukiendelea mbele zaidi twaweza sema kuwa dhambi ni pale ambapo
binadamu hukataa kuupoke ule upendo wa Mungu usio na kikomo. Kuna mwandishi
fulani wa vitabu aliyepata kusema kuwa kuna aina 700 za dhambi ambazo hata
hivyo zaweza kuwekwa kwenye makundi makuu matatu. Kundi la kwanza la dhambi ni
ile dhambi ya kutotii mamlaka ya Mungu. Mfano juu ya hili ni ile dhambi ya
Adamu na Hawa. Mungu aliwambia wasile tunda la mti wa kati, lakini wao kwa
kiburi chao wakakahidi hilo agizo."( Mwanzo 2: 15-17). Hii dhambi hata
nyakati zetu bado inaendelea kujidhihirisha. Huwa daima katika maisha
tunajikuta katika hali ambapo mmoja hupata kusema mimi najua kila kitu, mimi ni
mwanzo wa maarifa yote hivyo sihitaji kumsikiliza fulani au kufundishwa na
fulani. Lakini tunaalikwa daima kuwa watii kwa mamlaka, kwani mamlaka hupata
uweza na nguvu kutoka kwa Mungu.
Pili ni dhambi kati ya
ndugu kwa ndugu. Katika maandiko matakatifu tunapata kisa cha Kaini kumwua
ndugu yake Abel ( Mw4:8) katika hiki kisa chenye kuhudhunisha tunaona kuwa
Kaini anaamua kumtoa uhai ndugu yake kwa sababu ya chuki na wivu.
Kwa moyo wenye chuki, masengenyo na wivu katika maisha ya mkristu, huo moyo
yabidi usafishwe kwa sakramenti ya kitubio, kwani kumchukia mtu na kumdhamilia
vibaya huko ni kumwua.
Tatu, dhambi ya kuwa na
kiburi. Tunapata habari ya kisa cha kujengwa mnara wa Babel katika kitabu cha
agano la kale katika Biblia. ( Mw11:1-9). Kisa au historia hii inatuelezea
jinsi watu walivyokuwa wakaidi wakaamua kujenga mnara mrefu ili wafike pale Mungu
alipo. Huu mnara ni kilelezo cha mwanadamu kujitukuza, mwanadamu kujiona
anauwezo kama wa Mungu, mwanadamu kujifanya Mungu mbele ya wanadamu wenzake,
mwanadamu kujiona kuwa pasipoyeye mambo hayawezekani, na mwanadamu kupenda
kukaa juu ya wengine na kuwatawala pasipo ridhaa yao. Hao wajenga mnara
hawakuweza kumfikia Mungu kwa kuwa wao kwa wao hawakuweza kusikilizana, kuwa na
lugha moja na kauli moja. Vivyo hivyo katika maisha yetu daima hatuwezi kumwona
Mungu na kujua alipo pindi sisi wenyewe tukikosa kuwa wamoja na pia kuwa na
lugha moja ya kutuunganisha kama watoto wake. Daima kiburi ni sumu kubwa katika
mahusiano,kwani hakuna hata mmoja ambaye daima hudiliki kusemezana na wenye
majivuno. Kiburi daima huaribu urafiki kati ya watu. Daima upendo wa Kristu
hauwezi tawala maishani mwa kila mmoja wetu, pindi lugha ya mimi, baadala ya sisi, ninyi, na wao isipotawala katika maisha yetu.
Ndugu wapendwa daima
sote tunaalikwa kuwa wafuasi bora wa Kristu na siyo bora wafuasi. Daima
tunaalikwa kuiga mifano yake Bwana wetu Yesu Kristu. Kama yeye alitimiza
mapenzi yake Baba wa mbinguni kwa kufa msalabani basi nasi kwetu ni mwaliko
kuishi upendo wa namna hiyo hata kuwa tayari kutoa uhai wetu kwa ajili ya
wengine.